Rais wa Ufaransa Francois Hollande Jumamosi (06.12.2014) amekuwa
kiongozi wa kwanza wa Ulaya
kwenda Urusi kujaribu kupunguza mkwamo na
Vladimir Putin kuhusiana na Ukraine.
Wakati huo huo serikali mjini Kiev imetangaza duru mpya ya mazungumzo ya amani wiki ijayo.
Mkutano kati ya Hollande na Putin katika eneo la kidiplomasia katika
uwanja wa ndege nje ya mji mkuu wa nchi hiyo , umekuja wakati mzozo
katika eneo la mashariki mwa Ukraine umeporomosha uhusiano kati ya
mataifa ya magharibi na Urusi na kuwa katika kiwango chake cha chini
kabisa tangu wakati wa baada ya vita baridi.
Kiongozi huyo wa Ufaransa amesema ana matumaini ya kuzuwia mtengano
mwingine wa mataifa ya magharibi na mashariki na kwamba anamatumaini
kuona "matokeo mazuri " kutoka katika mazungumzo hayo na Putin, ambaye
mataifa ya Ulaya na Marekani yanamshutumu kwa kuwapa silaha na fedha
waasi mashariki mwa Ukraine.
Kutumia fursa
"Kuna wakati ambapo tunahitaji kutumia fursa. Huu ndio wakati.. nafikiri
tunapaswa kuzuwia kuta nyingine kututenganisha," amesema Hollande,
ambaye pia amezungumza na rais wa Ukraine Petro Poroshenko mapema jana.
"Tunapaswa kutafuta suluhisho kwa pamoja," amemwambia kiongozi huyo wa
Urusi, ambaye wiki hii ametoa hotoba ya kikakamavu akiyashutumu mataifa
ya magharibi kwa kuikandamiza Urusi.
Putin amesema kuna "matatizo magumu" kuyashughulikia lakini ziara hiyo ,
bila shaka itachangia katika suluhisho la matatizo mengi." Katika hatua
muhimu ya kukiri, Putin amesema kwa mara ya kwanza kwamba waasi
wanaoiunga mkono Urusi wamekiuka makubaliano tete ya kusitisha mapigano
na Ukraine.
"Tunaona kwamba pande zote mbili viongozi wa Ukraine na upande wa
viongozi wa Donetsk na Lugansk , kwa pande zote , si kila kitu ambacho
kimeheshimiwa," amewaambia waandishi habari baada ya mkutano ambao
umechukua karibu masaa mawili.
Ziara ya dakika za mwisho ya Hollande , ambayo chanzo kimoja katika
ujumbe wake kimesema pia ilikubaliwa na kansela wa Ujerumani Angela
Merkel , imekuja wakati Ukraine imetangaza duru mpya ya mazungumzo na
waasi mjini Minsk wiki ijayo kujaribu kuokoa makubaliano ya mwezi
Septemba yaliyovurugika ya kusitisha mapigano.
Mazungumzo mapya
Mazungumzo hayo yatafanyika siku ya Jumanne, pia tarehe hiyo imepangwa
na pande zote kwa ajili ya kupatikana makubaliano mapya ya kusitisha
mapigano.
Ukraine na waasi, ambao mapigano yao upande wa mashariki mwa nchi hiyo
yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 4,300 , wamekubaliana kusitisha
operesheni zao Desemba 9, na kuiita siku ya "ukimya".
"Katika muda wa siku 30 , pande hizo mbili zitawajibika kurejesha nyuma
silaha zao nzito kutoka katika eneo lisilotakiwa kuwa na mapambano ya
silaha lililoainishwa katika rasimu ya Minsk," Poroshenko amesema.
Kiongozi huyo wa Ukraine pia amesema kwamba pande zitakazokutana katika
mji mkuu wa Belarus zitalenga katika "kuthibitisha muda maalum
uliopangwa kutekeleza makubaliano ya mwanzo ya Minsk."
Makubaliano ya mwanzo yalizitaka pande zote kuacha kushambulia na
kuondoa silaha na majeshi yao, lakini yalifanikiwa tu kuzuwia ghasia
mbaya kutokea bila ya kusitisha machafuko kabisa.
0 maoni:
Chapisha Maoni