Alhamisi, 12 Machi 2015

TANZANIA ROAD SAFETY AMBASSADORS-RSA

(MABALOZI WA USALAMA BARABARANI)

TAMKO LA RSA KUHUSU AJALI NA HALI YA USALAMA BARABARANI

13.03.2015

Ndugu wananchi,

Napenda kuchukua nafasi hii, kwa niaba ya mabalozi wa usalama barabarani, kuungana na watanzania wote kutoa pole kwa wafiwa na majeruhi wa ajali ya basi la Majinja Express iliyotokea huko Mafinga mkoani Iringa tarehe 11.03.2015 kupoteza maisha ya watu 50 mpaka sasa na kuacha majeruhi wengi. Ajali hii ni ya kustua na kusikitisha sana. Poleni majeruhi na mwenyezi mungu awajalie majeruhi uponyaji wa haraka na marehemu awapokee kwenye nuru ya uso wake.

Kwa miaka mingi sasa ajali za barabarani zimeendelea kukatisha maisha ya watanzania walio wengi na kuwaacha wengi mayatima na ulemavu wa kudumu. Hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na serikali, lakini ufanisi wa hatua hizo bado umekuwa wenye mashaka. Imekuwa kawaida kuwa ajali inapotokea jibu la haraka limekuwa mwendo kasi na hatimaye tumeishia kutoa salamu za rambirambi tu na kusahau. Hatukatai ni kweli kabisa makosa ya kibinadamu inasemekana yanachangia sana hizi ajali. Hata hivyo ipo haja ya kwenda mbali zaidi ya majibu mepesi kuwa ni mwendo kasi. Katika ajali hizi daima suala la haki za majeruhi baada ya ajali limeendelea kuwa tatizo kubwa sana. Wengi wamekuwa hawapati haki zao kabisa au hupata kwa kuchelewa jambo linalopelekea kuwapa machungu zaidi majeruhi na hata yatima na wajane wanaobakia baada ya ndugu zao kufariki dunia. Ifike hatua tuache kutoa majibu mepesi kwa maswali magumu na kuchukua hatua stahiki ili kukabiliana na hali hii.

Sisi kama mtandao wa mabalozi wa usalama barabarani(RSA) tunaitaka serikali na wadau wanaohusika kuchukua hatua stahiki na za makusudi kukabiliana na hali hii hasa zinapotokea ajali kubwa(Major accidents).
  1. Kuundwa kwa taasisi huru na ya kitaalamu (Road Accidents Investigation Board) kuchunguza kwa kina ajali husika ili kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo na vitu vilivyochangia.
  2. Kuwaajibisha wote watakaobainika kwa namna moja ama nyingine kuchangia kusababisha ajali. Hii ihusishe uwajibikaji wa mamlaka mbalimbali kama vile Polisi Usalama Barabarani, SUMATRA, TANROADS na wamiliki wa magari husika.
  3. Bima za magari ya abiria na ya mizigo zichunguzwe ili kuona kama zinakidhi vihatarishi (Risks) vinavyoweza kusababishwa na magari hayo, uhai na uhalali wa bima hizo na ukubwa fidia zinazotolewa na bima hizo (coverage).
  4. Shule za udereva na sheria zake ziangaliwe upya ili kuona kama shule hizo zinakidhi mafunzo ya udereva kulingana na teknolojia ya sasa ya maendeleo ya magari na hasa mitaala inayotumika.
  5. Mfumo wa upatikanaji leseni uangaliwe kwa kina kuona kama hauna mianya ya kuwafanya watu wapate leseni bila kupitia mafunzo au kufuzu vizuri na ikiwezekana mamlaka inayojitegemea ya utoaji leseni na ukaguzi wa magari ianzishwe kama ilivyoainishwa kwenye sera ya usalama barabarani, 2009.
  6. Bodi ya uchunguzi wa ajali pamoja na mambo mengine ichunguze mambo yafuatayo na kuweka wazi ripoti yake:-  
  • Iwapo TANROADS wana programu ya ukaguzi wa mara kwa mara wa barabara na kuzifanyia marekebisho.
  • Iwapo mabasi yanayohusika kwenye ajali yanakuwa na Bima sahihi na inayotosha kufidia wahanga wa ajali hizo.
  • Iwapo kila mamlaka ilitekeleza wajibu wake kabla na baada ya kutokea kwa ajali, pawepo na bajeti ya kutosha kufanya matengenezo ya barabara na kama ipo kwanini ukaratabati haufanyiki kwa wakati.
  • Iwapo wamiliki wa mabasi wana sera na taratibu zozote za kukabiliana na ajali na nidhamu za watumishi wao.
  • Mafunzo ya dereva husika aliyepata ajali, historia ya maisha yake, na siku kabla ya ajali au wakati wa ajali hali ya akili yake ilikuwaje.
  • Nafasi ya hali ya kijiografia katika ajali husika mathalani, muundo wa kijiografia eneo hilo, hali ya hewa n.k
  • Mwendo wa gari husika na hali ya gari hadi wakati wa ajali (Roadworthiness).
  • Abiria kwa kiasi gani walichangia mwendo mbaya kwa kutoripoti na je iwapo waliripoti ni hatua gani stahiki zilichukuliwa dhidi ya dereva au abiria husika.
  7. Kutungwa kwa sheria ya mauaji ya bila kukusudia yanayosababishwa na taasisi (Cooperate            manslaughter Act) kama ilivyo nchini Uingereza ili kuziwajibisha taasisi zisizojali usalama wa watu.
  8. Kutekeleza kwa vitendo malengo ya sera ya usalama barabarani 2009, na kuweka adhabu kali kwa wanaokiuka sheria za usalama barabarani.
  9. Kuweka utaratibu mzuri wa kushughulikia malipo ya fidia ya bima kwa waathirika wa ajali ikiwemo wale wanaopata athari kutokana na magari ya serikali kusababisha ajali.
 10. Kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuelimisha na kuwaongezea abiria nguvu za kisheria za kudhibiti mwendo madereva njiani tunaamini haya yatatekelezwa vyema, tunaweza kupunguza ajali kwa kiwango kikubwa sana. 

Sisi kama mabalozi wa usalama barabarani tunaendelea kutii sheria bila shuruti na kuendelea kwa nguvu zetu zote kutoa elimu ya usalama barabarani kila siku kupitia mbinu mbalimbali.


Imetolewa na

JOHN SEKA
Kwa niaba ya Mabalozi wa usalama Barabarani- Tanzania

0 maoni:

Chapisha Maoni

Inaendeshwa na Blogger.

Machapisho Maarufu

Machapisho ya Karibuni

Recent Posts Widget