Leo Jumapili tarehe 12/04/2015, mwenyekiti wa taasisi ya wazalendo Taifa Ndg. Chief Daud Mrindoko ameyasema hayo katika uzinduzi wa Album ya Victor Mbagga ijulikanayo kwa jina la FURAHA KUWA NA YESU.
Fuatilia hotuba ya Chief Daud Mrindoko kuanzia mwanzo na mwisho:
HOTUBA YA MH. CHIEF DAUD BABU MRINDOKO KATIKA UZINDUZI WA ALBUM YA VICTOR MBAGGA TAREHE 12/04/2015: (UMOJA HOSTEL) MOSHI-KILIMANJARO.
Ndg. Victor Mbagga(mwibaji),
Ndg. viongozi wa dini,
Ndg. viongozi wa kwaya,
Ndg. waimbaji mbalimbali,
Wageni waalikwa, mabibi na mabwana:
Bwana yesu asifiwe, tumsifu yesu kristu;
Assalam Aleykum...!!!
Ndg. wageni waalikwa..
Naomba tuanze kumshukuru M/mungu kwa kutupa afya na uzima na kutuwezesha kukutana katika hafla hii ya uzinduzi wa Album ya kwaya ya ndg yetu. Kwani sio kwa ujanja wetu bali ni kwa nguvu zake M/mungu mwingi wa rehema.
Ni furaha yangu kuona wote tupo hapa na tumejumuika kwa umoja katika uzinduzi huu kwani ni furaha sana kwasababu ya amani aliyotujalia Mungu aliyetuwezesha kukutana hapa na kujumuika sote kwa pamoja.
Nilipopata mualiko huu kweli nilistuka sana kwakuwa sikutegemea mimi kuweza kupewa heshima kama hii, kwakuwa kuna watu wengi sana wenye uwezo mbalimbali na vyeo ambao wangeweza kualikwa kuwa miongoni mwa wageni rasmi. Lakini naamini mmenipa heshima kubwa sana kuweza kunialika mimi hapa na kujumuika nanyi ingawa sistahili. Basi kutokupenda kwenu makuu mkaona mnialike mie kuwa mgeni rasmi. Nawashukuru sana, kwani Mungu huvichagua vinyonge ili kjwashusha wenye nguvu, utukufu wake uonekane mbele za watu.
Ndg. wageni waalikwa, lengo la kuwa hapa ni kushiriki katika uzinduzi wa Album ya "FURAHA KUWA NA YESU" ya mwimbaji wetu Victor Mbagga.
Ndg. wageni waalikwa, kwaya hii ni yetu sote hivyo tujitahidi kuweza kuwawezesha hawa wanakwaya wenzetu kwa namna mbalimbali ikiwemo kwa kununja Album zao na kazi zao. Kwani kwa kufanya hivyo utapata faida kubwa kwa kuwa yale yanayo imbwa ndani ya nyimbo hizi za Injili ni ibada tosha na inatufanya tuweze kumwabudu na kumsifu Mungu wetu muumba wa mbingu na ardhi.
Vilevile tutakuwa tunawapa fursa wenzetu wanakwaya hawa kujiajiri na kuweza kuweza kujipatia kipato zaidi, kwani ukinunua kazi zao ndio wanajipatia kipato na fedha kuweza kuboresha zaidi na zaidi kazi zao za sanaa.
Ndg. wanakwaya, mimi binafsi naahidi niitawaunga mkono katika kazi yenu hii, na njtanunua kazi yenu. Lakini ninawaomba sana mjitahidi kuwa wabunifu ili kuboresha kazi zenu ziweze kushindana katika soko la kimataifa na kukubalika na watu wote, ili muweze kufikia katika viwango vya kimataifa lazima mkubali kuboresha kazi zenu na mfanye kazi kwa bidii kweli kweli ndio mtaweza kufanya vuzuri. Lakini mkibweteka hamtoweza kufanya vizuri katika anga za kimataifa.
Ndg. wageni waalikwa, ningependa kupitia jukwaa hili niweze kuwaomba mliombee taifa amani kwasababu tunaelekea katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa serikali kama mjuavyo uchaguzi mkuu huwa unagubikwa na hali ya kutishia uvunjifu wa amani, basi tuliombee sana taifa letu na pia tumuombee raisi wetu Prof. Jakaya M. Kikwete aweze kumaliza kipindi kilichobakia salama na tupate Rais mwingine mchamungu, mchapa kazi, mmoja wetu kutoka katika watu wenye utu wa kweli na uzalendo halisia.
Aidha, tupate wabunge na madiwani wenye kulijali taifa katika maeneo husika.
Kwakuwa, wabunge na madiwani hutokana na watu, hupendekezwa, kushawishiwa na kupigiwa kura na watu. Hivyo, suala la kupendekezwa na kushawishiwa linaanza kujitokeza ingawa muda bado. Mfano katika gazeti la Mwananchi la tarehe 08/03/2015 nilishangaa kuona watu Moshi manispaa wakinipendekeza kugombea kiti cha ubunge kwa kuongelewa hata kupigiwa simu na baadhi ya watu kunishawishi moja kwa moja. Walatini husema "VOX POPULI EST VOX DEI" yaani sauti ya watu ni sauti ya Mungu. Hivyo, nitajaribu kusikiliza sauti ya Mungu. Ndugu zangu, naomba sala zenu kwa mawazo, maneno na katika nyimbo zenu. Mungu atukuzwe!!!!
MWISHO:
Ndg. zangu mwisho kabisa naomba niwapongeze kwa mara nyingine tena wale wote waliohusika na maandalizi ya hafla hii na pia kuipongeza kwaya yetu hii na mwimbaji wetu Victor Mbagga, narudia tena kuwa nitawaunga mkono na tutashirikiana sote kwa pamoja kuhakikisha kwaya yetu hii inafanya vyema katika tasnia ya nyimbo za injili.
Ninawashukuru waimbaji wengine wote toka Kenya, Congo na Tanzania(wakiwemo Kilimanjaro, Arusha na Dsm).
Mungu awabariki sana,
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
Chief Daudi Babu Mrindoko.
0 maoni:
Chapisha Maoni