Wafungwa 6 waliokuwa wakishikiliwa na Marekani katika gereza la
Guantanamo Bay wamewasili nchini Uruguay, baada ya Marekani kuwapeleka
huko kama wakimbizi, katika hatua mpya za rais Obama kulifunga gereza
hilo.
Watu hao sita ambao walisafirishwa kwa ndege ya jeshi la Marekani, ndio
kundi kubwa zaidi kuwahi kuachiwa kwa pamoja kutoka gereza la Guantanamo
Bay ambalo linashutumiwa na jumuiya. Wanne miongoni mwao ni raia wa
Syria, mmoja ni kutoka Tunisia, na aliyebaki ni mpalestina.
Wote walituhumiwa kuwa wanamgambo wenye mafungamano na mtandao wa
kigaidi wa al-Qaida, lakini wameshikiliwa kwa muda wa miaka 12 bila
kufunguliwa mashitaka yoyote. Tangu mwaka 2009 walikuwa wameondolewa
mashitaka, lakini walibakia gerezani kwa sababu haikuwezekana
kuwarejesha nyumbani kwao, huku Marekani ikihangaika kupata nchi ya
kujitolea kuwapokea.Serikali ya Uruguay imethibitisha kuwasili kwa
wafungwa hao bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.
Pango la wateka nyara
Rais wa nchi hiyo Jose Mujica amesema nchi yake imekubali
kuwapokea watu hao kama wakimbizi kwa misingi ya kibinadamu, na kuahidi
kuwa muda wowote watakapojisikia kuondoka nchini humo wanao uhuru wa
kufanya hivyo mara moja. Rais Mujica pia ameikosoa Marekani na mfumo
wake wa kuwaweka watu katika kizuizi cha Guantanmo.
''Lile sio gereza bali ni pango la wateka nyara. Gereza huwajibika kwa
mfumo fulani wa sheria, na huwa na waendeshamashitaka wa aina moja au
nyingine, na majaji wowote wale. Gereza pia huendeshwa kwa mfumo fulani
wa sheria. Kule hakuna chochote.'' Amesema rais Mujica.
Alipochukua madaraka miaka sita iliyopita rais Obama aliahidi kulifunga
gereza hilo, akisema limeitia doa sura ya Marekani machoni mwa dunia
nzima. Hata hivyo muda huo wote ameshindwa kutekeleza azma yake hiyo,
hasa kutokana na upinzani wa bunge la nchi yake.
Changamoto za kuifunga Guantanamo
Kwa wakati huu Marekani inawashikilia wafungwa wengine 67 ambao
wameruhusiwa kuondoka, ambao hata hivyo kama wenzao sita waliopokelewa
sasa na Uruguay hawana pa kwenda, wakihofia mashitaka iwapo watarudi
katika mataifa yao, au wakihofia usalama wao.
Mjumbe wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Clifford Sloan
ameisifu Uruguay na rais wake Jose Mujica kwa kile alichokiita ''uongozi
wake imara wa kuwapa hifadhi watu ambao hawawezi kurudi kwao''.
Wakili wa mmoja wa wa watu hao waliopokelewa na Uruguay Ramzi Kassem
amesema kwa kuwapokea watu hao kama binadamu huru, nchi hiyo ya Amerika
Kusini imedhihirisha kwa vitendo, msimamo wake wa kishujaa.
Uruguay tayari imekwishawapokea wakimbizi wengine 42 kutoka Syria, na
imesema itawapokea wengine 80. Mkurugenzi wa kituo cha kiislamu nchini
Uruguay Tamar Chaky, amesema Uruguay imefanya ukarimu huo licha ya
kwamba huenda ni nchi pekee ya Amerika Kusini isio ya msikiti hata
mmoja.
Kwa wakati huu gereza la Guantanamo linabaki na wafungwa 136, ambayo ni
idadi ndogo zaidi tangu lilipofunguliwa mwaka 2002. Mnamo siku 30
zilizopita Marekani imeweza kuwaondoa wafungwa wapatao 30 katika gereza
hilo.
0 maoni:
Chapisha Maoni