MBUNGE wa Vunjo ambaye pia ni Mjumbe
wa Bunge Maalum la Katiba, Augustine
Mrema (TLP), amesema kuna haja Rais
Jakaya Kikwete aongezewe muda wa
kuongoza nchi.
Alisema kama Rais Kikwete ataongezewa
muda, atapata muda wa kukamilisha
mchakato wa Katiba ambao ndiye
aliyeuanzisha.
Mmoja wa wajumbe waliohudhuria kikao
kati ya Rais Kikwete na Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) kilichofanyika
mwanzoni mwa wiki Ikulu ndogo ya
Kilimani mjini Dodoma, aliiambia
MTANZANIA JITAMBUE kwamba Mrema aliyasema
hayo alipokuwa akichangia wakati wa
kikao hicho.
“Wakati mjadala unaendelea, Mrema
alipendekeza Rais Kikwete aongezewe muda
wa mwaka mmoja au miwili ili afanikiwe
kukamilisha mchakato huu wa Katiba.
“Alipotoa pendekezo hilo, kuna mjumbe
mmoja akamuuliza, ‘sasa Mrema unataka
muda uongezwe ili na wewe upate muda
wa kupambana na Mbatia (James
Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi)
anayekusumbua kule Vunjo au?’
“Huyo mjumbe alipouliza hivyo, Mrema
akadakia na kusema, ‘hapo hapo’,” kilisema
chanzo chetu kwa sharti la kutotajwa .
Chanzo hicho kilisema kuwa Mrema
aliendelea kumsihi Rais Kikwete amzuie
Mbatia asiende Vunjo kwa kuwa anapokuwa
huko anatumia jina lake, kwamba
amemtuma kugombea ubunge wa jimbo
hilo.
Mbatia alipozungumza na MTANZANIA JITAMBUE kwa
simu jana juu ya malalamiko hayo, alisema
hawezi kuendelea kujibizana na Mrema
kwa kuwa ni mkubwa wake.
“Mimi sikulelewa katika mazingira ya
kujibizana na wakubwa zangu ila
ninachosema ni kwamba, wakati wa mkutano
wangu wa hadhara niliohutubia Vunjo wiki
iliyopita, wenyeviti 11 wa serikali za vijiji
walioshinda kupitia TLP, wenyeviti 32 wa
vitongoni ambao ni wa TLP, msaidizi wa
Mrema pamoja na wanachama wapya 1,564,
walihamia NCCR-Mageuzi,” alisema Mbatia.
Naye Mrema alipozungumza na
MTANZANIA JITAMBUE kwa simu, alikiri kutaka Rais
Kikwete aongezewe muda na kumwomba
amzuie Mbatia kwenda Vunjo akidai kuwa
anatumia jina la rais kumsema vibaya kwa
wananchi.
Ijumaa, 12 Septemba 2014
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
0 maoni:
Chapisha Maoni